Na George Ramadhan,Mwanza.
WILAYA ya Kwimba mkoani Mwanza imekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa mafua ya nguruwe ambapo watu 142 wakiwemo wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Ilula wamethibitika kuugua ugonjwa huo.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk.Meshack Massi amewaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa mlipuko wa ugonjwa huo ulianza Novemba 19 kwa jumla ya wanafunzi 56 wa shule ya msingi Ilula kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Alizitaja dalili hizo kuwa homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo, maumivu ya misuli na uchovu, kikohozi, mafua, maumivu ya koo, kuhisi baridi na kutetemeka pamoja na kukosa hamu ya kula.
Alisema kwamba baada ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo kuona dalili hizo alitoa taarifa ambapo sampuli zilichukuliwa na kupelekwa jijini Dar es salaam kwa uchunguzi zaidi na majibu yamethibitisha kuwa ni ugonjwa wa mafua ya nguruwe.
Kwa mujibu wa Dk.Massi, baada ya wagonjwa 56 wa kwanza, siku ya pili walibainika wagonjwa wengine 30, siku ya tatu wagonjwa 8, siku ya nne wagonjwa 7, siku ya tano wagonjwa 30, siku ya 6 wagonjwa wanane na siku ya 7 waliongezeka wagonjwa wengine watatu.
Aliongeza kwamba miongoni mwa wagonjwa hao wamo wanafunzi, walimu na wakazi wengine wa kijiji cha Ilula lakini akasema kuwa mchanganuo unaoonyesha idadi kamili ya wanafunzi, walimu, wanakijiji na jinsi zao ingepatikana baadaye.
Alisema kuwa uchunguzi unaonyesha ugonjwa huo ulianzia kwa mwanafunzi mmoja ambaye baba yake ni mfanyabishara wa kuuza kuku anayesafiri mikoa mbalimbali hivyo inaaminika kuwa pengine ndiye aliyeleta wadudu wa ugonjwa huo na kusababisha mlipuko.
Hata hivyo alisema kwamba tayari wagonjwa wote wamepewa dawa zilizotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii huku wakiwa chini ya uangalizi katika vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Ilula.
Dk.Massi alisema kwamba kufuatia kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa huo imelazimu shule ya msingi Ilula kufungwa kwa muda ili kutoa fursa kwa madarasa ya shule hiyo kutumiwa kama kambi ya wagonjwa wanaoendelea kupatiwa matibabu.
Ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari kwa kuepuka kukaribiana na wagonjwa lakini pia kwa kujifunga vitambaa puani na mdomoni ili kuepuka kuambukizwa ugonjwa huo.
Aidha aliwataka wananchi pindi wanapokohoa, kupiga chafya au kupiga miyayo kuhakikisha wanaziba midomo yao kwa vitambaa ili kuepuka kusambaa kwa wadudu wanaosababisha homa ya mafua ya nguruwe.
Gazeti la Nipashe Jumapili ndilo lilikuwa la kwanza kuripoti juu ya wanafunzi wa shule ya msingi Ilula kuugua ugonjwa usiojulikana baada ya jumla ya wanafunzi 56 pamoja na mwalimu mmoja kulalamika maumivu ya kichwa na kupiga makelele.
Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kwimba Boaz Pius alisema kwamba baada ya kufanyiwa vipimo vya awali wanafunzi hao walibainika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa malaria ambapo walitibiwa lakini wanne kati yao hali zao zilikuwa mbaya hivyo kulazimika kupumzishwa katika zahanati ya eneo hilo .
Mwisho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment